Liturujia ya Vipindi ni sala rasmi ya Kanisa kama inavyoadhimishwa katika madhehebu mbalimbali ya Ukristo, lakini ni jina hasa la mpangilio unaofuatwa na Kanisa la Roma baada ya Mtaguso wa pili wa Vatikano (kwa Kilatini jina ni Liturgia Horarum).
Kwa njia yake wakleri, watawa na waamini wote wa Yesu wa madhehebu hayo wanaungana naye katika sala yake ya kudumu, na wanasaidiwa kuishi kitakatifu saa zote za siku kwa kumkumbuka Mungu mara kwa mara.
Inaitwa hivyo kwa sababu inafanyika kwa vipindi mbalimbali kadiri ya mwendo wa siku (usiku na mchana): muhimu zaidi ni vipindi vya asubuhi (Masifu ya asubuhi) na jioni (Masifu ya jioni), lakini kuna pia vipindi vya usiku kati au alfajiri (Kipindi cha masomo), mchana (Sala ya kabla ya adhuhuri, Sala ya adhuhuri na Sala ya baada ya adhuhuri) na kabla ya kulala (Sala ya mwisho).
Katika Kanisa la Kilatini hiyo sala ya Kanisa inategemea hasa Biblia ya Kikristo kwa kutumia Zaburi na masomo kutoka kwake.
Matini yake yote yamekusanywa pamoja katika kitabu kimoja ambacho kwa sababu hiyo kilizoeleka kuitwa breviari (yaani: "matini kwa ufupi", badala ya kuzagaa katika vitabu mbalimbali kama zamani).
© MMXXIII Rich X Search. We shall prevail. All rights reserved. Rich X Search