Qurani Tukufu

Inaelekeza kwa:

Historia ya Uandishi wa Qurani

Qurani Tukufu, kwa mujibu wa Waislamu, imeteremshwa na Mwenyezi Mungu kupitia Jibrili mmojawapo wa Malaika wakubwa wenye heshima kubwa huko mbinguni. Qurani iliteremka kwa njia ya Wahyi au Ufunuo katika muda wa miaka 23 ya Utume wa Muhammad. Maneno yote yaliyokuwemo ndani ya Qurani yanadaiwa na Waislamu kuwa ni ya Mwenyezi Mungu na kuwa Muhammad hakuwa akisema maneno haya kwa mujibu wa matamanio yake.

Qurani Tukufu ilikuwa ikiteremshwa kidogo kidogo katika muda huu wa miaka 23 kulingana na munasaba mbali mbali wa maisha ya Waislamu wa wakati huo ili kuwafahamisha namna bora ya kuishi ulimwenguni kwa wema na hisani na uhusiano wao baina yao wenyewe kwa wenyewe na baina yao na wasiokuwa Waislamu katika wao. Aidha, Qurani ilikuwa ikigusia masuala mbali mbali ya maisha na mifano ya umma zilizopita ambazo hazikukubali tume za Mwenyezi Mungu kwao na kuangamizwa kwao kwa kupinga na kwenda kinyume na Mitume na Manabii wao.

Zama za Mtume Muhammad

Qurani Tukufu ilipoteremka kwanza iliandikwa, kwa amri ya Mtume Muhammad, kwenye vitambaa, ngozi, mifupa na majiwe. Muhammad alikuwa akiwaelekeza waandishi wake waandike kwa mujibu wa mpango na utaratibu fulani ambao unatokana na Mwenyezi Mungu mwenyewe. Katika wakati wa Mtume Muhammad Qurani ilikuwa zaidi katika nyoyo za Masahaba ambao wengi wao walikuwa wameihifadhi Qurani nzima, na wengi wao walikuwa wakiiandika kwa njia mbali mbali lakini ilikuwa si katika msahafu mmoja.

Zama za Abubakar Siddiq

Katika zama za Abubakar Siddiq, Khalifa wa Mtume wa kwanza baada ya kufa kwake, alimtuma Zayd bin Thabit kuikusanya Qurani yote katika Kitabu kimoja. Umar bin Al-Khattab, Khalifa wa pili ndiye aliyemshauri Abubakar kuikusanya Qurani na ijapokuwa mwanzo aliona taabu kufanya jambo ambalo Mtume mwenyewe hakulifanya. Hatimaye, Abubakar alikubali rai yake na Qurani ikakusanywa katika kitabu kimoja.

Zama za Uthman bin Affan

Baada ya Qurani kuandikwa kamili katika msahafu mmoja na kuwekwa katika nyumba ya Hafsa bint Umar, mmoja katika wakeze wa Mtume Muhammad, ulipofika wakati wa kutawala Uthman bin Affan, Khalifa wa tatu wa Mtume Muhammad, aliamrisha waandishi fulani kuuchukuwa huo msahafu na kunukulu nakala nyengine kwa ajili ya kupeleka sehemu mbali mbali za ulimwengu wa kiislamu ambao kwa wakati huo ulikuwa umekuwa mkubwa sana na kufikia nchi nyingi za Afrika na Asia na Ulaya.

Waandishi wa Qurani Tukufu

Uthman bin Uffan aliwaamuru waandishi wafuatao kuandika Qurani kutoka na msahafu wa Hafsa na kutawanya nakala hizi katika sehemu mbali mbali za ulimwengu wa kiislamu.

Zayd Ibn Thabit. Abdullah Ibn Al-Zubair. Said Ibn Al-`As. Abdul-Rahman Ibn Al-Harith Ibn Hisham.

Uthman aliweka nuskha moja Madina na kupeleka nyenginezo sehemu nyenginezo za ulimwengu wa kiislamu.


© MMXXIII Rich X Search. We shall prevail. All rights reserved. Rich X Search