Ufalme

Taji la mfalme Louis XV wa Ufaransa; taji ni alama za cheo cha mfalme katika nchi nyingi

Ufalme ni mfumo wa utawala ambapo mfalme, malkia au mtu mwingine aliyerithi cheo chake ni mkuu wa dola. Vyeo vingine vya mkuu katika ufalme ni pamoja na kaisari, shah, tenno, sultani, amiri au mtemi. Kwa kawaida mfalme amerithi cheo chake kutoka kwa baba yake au mama yake, kwa hiyo alizaliwa kama mfalme mteule na ataendelea kuwa na cheo hicho hadi kifo chake. Lakini kama mfalme aliyetangulia hakuwa na mrithi inawezekana ya kwamba mfalme mpya amechaguliwa. Mfano wa dola lenye mfumo wa ufalme ambapo mkuu anachaguliwa mara kwa mara ni Vatikani ambapo Papa ni mkuu wa dola.

Neno ufalme hutumiwa pia kwa kutaja nchi inayotawaliwa na mfalme au malkia, kwa mfano Ufalme wa Maungano, Ufalme wa Eswatini na kadhalika.

Kiwango cha madaraka cha mfalme huwa na tofauti kubwa. Leo hii wafalme wengi wako chini ya katiba ya nchi na mara nyingi wana madaraka machache; nafasi yao ni ya heshima na desturi. Lakini kuna falme kadhaa ambaPo mfalme bado ana madaraka makubwa, habanwi na katiba wala bunge wala serikali kama vile Omani au Saudia.


© MMXXIII Rich X Search. We shall prevail. All rights reserved. Rich X Search