Dhambi

Dhambi (kutoka Kiar. ذنب dhanaba kukosa, kutenda dhambi au jinai[1]) ni kosa la kiumbehai mwenye hiari dhidi ya uadilifu unaompasa.

Inaweza kufanyika kwa mawazo, maneno, matendo na kwa kutotimiza wajibu.

Maadili yanamuelekeza binadamu katika kutambua dhambi ni zipi pamoja na madhara yake.

Kwa kawaida dini zinahusianisha kosa hilo na Mungu aliye asili ya uadilifu, kwa kuwa ndiye aliyeumba viumbe vyote na kuvielekeza maishani.

Akiwapa baadhi ya viumbehai akili na utashi, papo hapo Mungu amewapa wajibu wa kufuata maelekezo yaliyomo katika utaratibu wa nafsi yao na wa ulimwengu wote.

Katika dini zinazofundisha kwamba Mwenyezi Mungu alitoa ufunuo wake hata kwa njia ipitayo maumbile, ni dhambi kwenda kinyume cha ufunuo huo, kwa mfano unavyopatikana katika vitabu vitakatifu vya dini husika, kama vile Biblia kwa Wayahudi na Wakristo na Kurani kwa Waislamu.

Kutokana na uenezi wa dhambi kuanzia dhambi ya asili, linajitokeza suala la wokovu, ambalo linaweza kutazamwa zaidi kama neema, lakini kwa kawaida linadai toba ya mkosefu.

Kanisa Katoliki na hata baadhi ya madhehebu mengine ya Ukristo linaamini linaweza kuondolea dhambi yoyote katika ubatizo na kitubio kwa kutumia mamlaka ambayo Yesu mfufuka aliwashirikisha Mitume wake alipowavuvia akisema: “Pokeeni Roho Mtakatifu. Wowote mtakaowaondolea dhambi, wameondolewa; na wowote mtakaowafungia dhambi, wamefungiwa” (Yoh 20:22-23). “Mlikuwa watu wa namna hii; lakini mlioshwa, lakini mlitakaswa, lakini mlihesabiwa haki katika jina la Bwana Yesu Kristo, na katika Roho wa Mungu wetu” (1Kor 6:11).

  1. Linganisha kamusi ya Krapf (1882), "thambi".

© MMXXIII Rich X Search. We shall prevail. All rights reserved. Rich X Search