Lugha za Kibantu

Ramani hii inaonyesha enezi la lugha za Kibantu (rangi ya machungwa) kulingana na lugha nyingine za Niger-Congo (rangi ya manjano).

Lugha za Kibantu ni kundi la lugha ambalo ni tawi la lugha za Niger-Kongo.

Lugha za Kibantu huzungumzwa hasa katika nchi za Nigeria, Kamerun, Guinea ya Ikweta, Gabon, Jamhuri ya Kongo, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Rwanda, Burundi, Uganda, Kenya, Tanzania, Komori, Msumbiji, Malawi, Zambia, Zimbabwe, Angola, Namibia, Botswana, Lesotho, Eswatini na Afrika ya Kusini.

Uenezi huo unaonyesha kwamba kundi la lugha za Kibantu ni kubwa kabisa barani Afrika, na idadi ya wanaozitumia ni takriban watu milioni 310.

Neno Bantu, maana yake ni watu katika lugha nyingi za kundi hilo. Shina lake ni -ntu, na kiambishi awali cha ba- kinaonyesha uwingi wa viumbehai. Kwa sababu hiyo, mtaalamu Wilhelm Heinrich Immanuel Bleek (aliyeishi tangu mwaka 1827 hadi 1875) alitumia neno hilo kwa kurejea kundi la lugha hizo. Bleek alilinganisha sarufi za lugha mbalimbali za Kibantu, na baadaye Carl Meinhof alimfuata katika utafiti huo.

Kuna mamia ya lugha za Kibantu; wataalamu wengine wanahesabu 300, wengine wanahesabu 600. Mtaalamu Malcolm Guthrie aliziainisha kulingana na maeneo ya kijiografia. Kila eneo limepata herufi yake — A, B, C, D, E, F, G, H, K, L, M, N, P, R na S — na ndani ya kila eneo kuna tarakimu tena. Pia, Guthrie alichunguza lugha ya nasaba ambayo ni chanzo cha lugha zote za Kibantu.


© MMXXIII Rich X Search. We shall prevail. All rights reserved. Rich X Search