Tohara

Tohara inavyofanyika.
Ndivyo ilivyo kabla na baada ya tohara
Uenezi wa tohara duniani.

Tohara (kutoka Kiarabu: طهارة tahara - safi, tahiri) ni upasuaji mdogo wa kukata na kuondoa govi, yaani ngozi inayofunika ncha ya uume.

Wakati mwingine ukeketaji huitwa "tohara ya mwanamke", lakini matumizi hayo si sahihi, kwa sababu ni aina tofauti za upasuaji, ingawa zote mbili zinahusu viungo vya uzazi.

Tohara inaweza kufanyika katika umri wowote na kwa sababu za kiutamaduni, za kidini au za kiganga. Mara nyingi desturi za kutahiri zinachanganya sababu za kidini na za kiutamaduni. Kwa mfano, Waislamu wa Misri huamini ya kwamba wanatahiri watoto wao kama amri ya kidini lakini Wakristo Wakopti wa nchi hiyo hutahiri watoto vilevile. Ukweli ni kwamba tohara ilikuwa desturi ya Wamisri tangu kale.

Tohara inafanyika hasa mara baada ya kuzaliwa kwa mtoto au wakati wa kubalehe.

Kufuatana na Shirika la Afya Duniani takriban 30% za wanaume wote duniani wametahiriwa, wengi wao wakiwa Waislamu.


© MMXXIII Rich X Search. We shall prevail. All rights reserved. Rich X Search