Uhai

Uhai (kutoka neno la Kiarabu; pia uzima; kwa Kiingereza: life) kwa maana ya biolojia ni jumla ya tabia zinazotofautisha kiumbehai na mata kwa jumla. Hata hivyo kila uhai ulioweza kuchunguzwa na sayansi unapatikana pamoja na mata.

Kati ya tabia hizo kuna uwezo wa kushawishiwa na mazingira, kujipanga, kukua, metaboli na kuzaa. Kila tabia peke yake haifanyi uhai, kwa sababu mojamoja zinaweza kutokea pia kwa mata isiyo hai: fuwele zinakua, ulimi wa moto una umbo maalumu na ndani yake kuna aina ya metaboli inayobadilisha molekuli za nta pamoja na oksijeni ya hewani dioksidi kabonia na maji. Kwa hiyo ni jumla ya tabia zinazothibitisha uwepo wa uhai, lakini hadi leo wataalamu hawajapatana bado ni masharti gani yanayohitajika, kwa sababu kuna tofauti kati ya viumbehai ambazo hazifanani katika tabia zote kwa pamoja.

Uhai unapatikana kwa umbo la viumbehai wanaopangwa katika vikundi vinavyofanana kati yao. Kila kiumbehai hufanywa na vitengo hai ndani yake vinavyoitwa seli.


© MMXXIII Rich X Search. We shall prevail. All rights reserved. Rich X Search